Home PAHALA PANO NI PAPI

PAHALA PANO NI PAPI

Mashariki pambazuka, la kwako jua
nilone
Nisije shida kumbuka, chembechembe
wala tone
Kiza kipate toweka, mwanga kiza
utafune
Pahala pano ni papi, mwanga wapi
mejificha?

Mwanga wapi mejificha, nakungojele
upenye
Hata lini kutakucha, nakwombele
sinisinye
Dunia sikawe bucha, mulika vita ufinye
Pahala pano ni papi, mbona mbele
nyuma sawa?

Mbona mbele nyuma sawa, bonde
milima yacheka
Tangu damu kuiuwa, mizoga sasa
twazika
Mbayasiasa tambuwa, katuacha
kachanika
Pahala pano ni papi, ndugu baba
mama wapi?

Ndugu baba mama wapi, kupi
wamepoteleya
Kuwamaliza siapi, japo walinilemeya
Kunirusha kama napi, wangu wema
katemeya
Pahala pano ni papi, tafadhali nelezeni

Tafadhali nelezeni, nani huyo anasema
Soko hadi kanisani, potepote pawe
pema
Siasa shakuwa duni, na gizani
metutema
Pahala pano ni papi, na vipi
tutabanduka?

Na vipi tutabanduka, tena vipi tutatoka
Lini tutamakinika, tusite kusikitika
Lini tutaimarika, uchumi kutozamika
Pahala pano ni papi, uongozi huno
upi?

Uongozi huno upi, mbona hauelekezi?
Migogoro hino ipi, mbona hamnielezi?
Umoja wetu uwapi, amani kila kizazi
Pahala pano ni papi, mwanga mulika
tupone

Mwanga mulika tupone, tusahau
yalopita
Langu kabila Silone, na chuki yache
kukita
Taifa na tupendane, siasa silete vita
Pahala pano ni papi, tupatoke twende
mbele

Tupatoke twende mbele, yetu nchi
tuijenge
Ngumi kofi na tekele, ukabila tuupinge
Naiona sa miale, mfisadi sijiringe
Pahala pano ni papi, virago
ninapofunga

Virago ninapofunga, himizo kwetu
naacha,
Amani anza kuchunga, ukabila chuki
acha,
Haki na ukweli funga, kiunoni sije
chacha,
Pahala pano ni papi, kwaheri mi
naondoka

© Peter Pages Odhiambo

courtesy of Storyzetu

0 Responses

  1. Masido says:

    Wah!hands down!i love ths shairi. I cant get enough of Swahili poetry. Me want another wrap!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Subscribe to our newsletter

Click Subscribe to get our latest news and stories straight to your email

Hello

Subscribe to our newsletter